Umoja wa Mataifa watoa wito wa msaada wa haraka kuepuka ukame unaosababisha njaa nchini Somalia
2022-06-08 08:52:07| CRI

Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Adam Abdelmoula ametoa wito wa msaada wa haraka wa kimataifa wakati baa la njaa linalosababishwa na ukame likitishia maisha ya maelfu wa watu nchini Somalia.

Akizungumza na wanahabari katika Makao Makuu ya Umoja huo mjini New York, Marekani, Abdelmoula amesema Somalia iko hatarini kukumbwa na baa la njaa linaloweza kusababisha vifo vya maelfu ya watu. Ameongeza kuwa, tangu mwanzo wa mwaka huu, hali ya ukame nchini Somalia imekuwa mbaya zaidi , na kwa sasa inakaribia kuwa janga kubwa.

Amesema, hivi karibuni baadhi ya sehemu nchini humo zilipata mvua kiasi, lakini hazikutosha kuondoa hali mbaya ya ukame, na kuonya kuwa, kuna hatari kuwa msimu ujao wa mvua pia utakuwa chini ya kiwango, na kuashiria mwaka wa tano wa uhaba wa mvua.