Mauzo ya bidhaa za Kenya barani Afrika yaongezeka kwa asilimia 20 katika robo ya kwanza mwaka huu
2022-06-09 10:23:46| CRI

Mauzo ya bidhaa za Kenya kwa nchi nyingine za Afrika yameongezeka kwa asilimia 20 katika robo ya kwanza ya mwaka huu, kufuatia juhudi za nchi hiyo kupanua uhusiano wake wa kibiashara na nchi nyingine za Afrika.

Takwimu zilizotolewa na Benki Kuu ya Kenya zinaonyesha kuwa, mauzo hayo yaliongezeka kutoka dola milioni 587 za kimarekani katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 hadi dola milioni 702 za kimarekani katika katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Mauzo kwa nchi za Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yamechangia zaidi ongezeko hilo. Kenya ilisaini makubaliano mbalimbali ya ushirikiano na DRC mwaka jana, na pia imeanzisha tume ya kibiashara ili kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili. Aidha, mwezi Desemba mwaka jana, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenzake wa Tanzania Samia Suluhu Hassan walisaini makubaliano kadhaa ili kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.