Mauaji yanayotokana na ugaidi yapungua duniani lakini yaongezeka Afrika
2022-06-09 08:40:58| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, idadi ya vifo vinavyotokana na mashambulizi ya kigaidi duniani imepungua lakini inaongezeka barani Afrika.

Akizungumza jana jumatano katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Uratibu wa Kupambana na Ugaidi, Bw. Guterres amesema eneo la Sahara barani Afrika limechukua asilimia 48 ya vifo vinavyotokana na mashambulizi ya kigaidi duniani kwa mwaka jana. Ameongeza kuwa, makundi ya kigaidi kama al-Qaida, IS na washirika wake yameendelea kukua katika eneo la Sahel na kupenyeza katika maeneo ya Afrika ya Kati na Kusini.

Amesema makundi hayo yanatafuta kutumia fursa za malalamiko na jamii kukosa imani na serikali zao katika nchi zenye amani kama vile Msumbiji na Tanzania.

Katibu mkuu huyo ameeleza matarajio yake kutokana na ziara yake katika jimbo la Borno nchini Nigeria, ambalo awali lilikuwa ngome ya kundi la Boko Haram, ambalo kwa sasa liko katika mchakato wa maafikiano na kurejeshwa upya katika jamii.