Somalia na UM waanza kampeni ya chanjo ya kipindupindu
2022-06-15 08:34:40| CRI

Somalia na mashirika ya Umoja wa Mataifa wameanza kampeni ya siku tano ya kutoa chanjo ya kipindupindu kwa watu laki 9.3 kwenye maeneo tisa yenye hatari kubwa ya maambukizi ambayo yanakabiliwa na mlipuko wa ugonjwa huo.

Wizara ya Afya na washirika wake wakiwemo Shirika la Afya Duniani WHO na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, wamesema raundi ya kwanza ya utoaji wa chanjo ya matone inalenga kuwachanja watu wakiwemo watoto wenye umri wa zaidi ya mwaka mmoja, wajawazito na wakimbizi wa ndani.

Somalia imeshuhudia milipuko kadhaa ya kipindupindu tangu mwaka 2017, kutokana na idadi kubwa ya watu kukosa maji safi na huduma za usafi, pamoja ya majanga ya asili, ikiwemo ukame na mafuriko, ambavyo vimechochewa na mgogoro wa muda mrefu na idadi kubwa ya wakimbizi.