Msichana mmoja wa Nigeria aliyetekwa nyara na kundi la Boko Haram miaka minane iliyopita kutoka kwenye shule yake katika jimbo la Borno, amepatikana Jumanne wiki hii wakati wanajeshi wakifanya doria katika mji wa Ngoshe wa jimbo hilo.
Msichana huyu ambaye sasa ni mtu mzima amegunduliwa na mwanaye mmoja na wanajeshi wa kikosi cha 26 cha nchi hiyo, na anaaminika kuwa mmoja kati ya wasichana 276 waliotekwa nyara na Boko Haram kutoka shuleni huko Chibok Aprili 14, 2014.
Tukio hilo la utekaji lilichochea ufuatiliaji mkubwa wa kimataifa ukitaka wasichana hao kuachiwa huru. Hapo awali baadhi ya wasichana waliokolewa na wanausalama au waliachiwa baada ya mazungumzo kati ya serikali na kundi la Boko Haram, lakini wengi wao bado hawajapatikana.