China na Kenya zakubaliana kuimarisha ushirikiano
2022-06-16 08:38:31| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Wang Yi amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa Kenya Bibi Raychelle Omamo, na wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zao.

Akiitaja Kenya kuwa mshirika wa kimkakati wa China, Bw. Wang amesema chini ya mwongozo wa wakuu wa nchi hizo mbili, uhusiano kati ya China na Kenya umeingia kwenye kipindi kizuri zaidi katika historia, huku kiwango cha kuaminiana kisiasa kikiendelea kuinuka na ushirikiano wa kiutendaji kati ya nchi hizo mbili ukiongoza njia ya ushirikiano wa jumla kati ya China na Afrika.

Bw. Wang amesema China iko tayari kushirikiana na Kenya katika kutetea na kutekeleza mfumo wa pande nyingi, kulinda maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea, na kushikilia kanuni za msingi zinazoongoza mahusiano ya kimataifa. Ameongeza kuwa China inatarajia ushiriki wa Kenya kwenye Mpango wa Maendeleo Duniani (GDI).

Bibi Omamo amesema China ni mshirika muhimu wa Afrika, na kwamba Kenya na nchi nyingine za Afrika zinapenda kushirikiana na China kwenye kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC, na pia Kenya inaunga mkono mpango wa GDI.