Serikali ya Tanzania yahimizwa kutumia nishati safi kwenye magari ili kupunguza uchafuzi
2022-06-17 09:00:31| CRI

Bunge la Tanzania limetoa mwito kwa serikali ifanye mabadiliko kwenye magari yake yote yanatotumia mafuta na kuanza kutumia gesi asilia kwa ajili ya kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa na kuokoa gharama.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge inayoshughulikia bajeti Bw. Sillo Baran alisema japo Tanzania ina maliasili nyingi ikiwa ni pamoja na gesi asilia, bado imebaki nyuma katika kutumia maliasili hizo kuhimiza maendeleo na kupambana na umaskini. Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje.

Habari zinasema Chuo cha Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT)  kinachoendeshwa na serikali kinashiriki katika kazi ya ubadilishaji huo. Kazi hiyo ilianza mwaka 2018, na hadi sasa DIT imebadilisha magari zaidi ya 800 yaliyotumia mafuta kuwa ya kutumia gesi ambapo watu wengi zaidi sasa wanapulizia kuhusu kufanya mabadiliko kwenye magari yao.