Tatizo la usalama wa chakula ni changamoto kubwa inayoikabili Afrika
2022-06-20 10:11:23| CRI

Leo tarehe 20, Juni ni Siku ya Wakimbizi Duniani. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa kwa pamoja na Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa WFP na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, katika miaka kumi iliyopita, idadi ya wakimbizi katika kanda ya Afrika Mashariki imeongezeka kutoka milioni 1.82 hadi milioni 5 ya sasa, ambapo katika mwaka jana pekee, idadi hiyo iliongezeka kwa laki tatu.

Juu ya hali hii, mtaalamu wa masuala ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani USIU jijini Nairobi Kenya profesa Macharia Munene alisema mafuriko na maafa makubwa ya ukame yametokea mara kwa mara, na kusababisha usalama wa chakula katika nchi kama Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini na Sudan, hivyo watu wengi wamelazimika kukimbia makazi yao ili kutafuta mahali penye maji na chakula.

Profesa Munene amesema tatizo la usalama wa chakula ni changamoto kubwa inayoikabili Afrika, na kama halitatatuliwa ipasavyo, idadi ya wakimbizi itaendelea kuongezeka. Ameongeza kuwa nchi nyingi za Afrika zinategemea kuagiza chakula kutoka nje, lakini vikwazo vilivyowekwa na nchi za magharibi zinazoongozwa na Marekani dhidi ya Russia vimeongeza makali ya tatizo la usalama wa chakula barani Afrika na hata dunia nzima.