Kenya yarejesha utaratibu wa kuvaa barakoa baada ya maambukizi ya UVIKO-19 kuongezeka
2022-06-21 09:47:28| CRI

Wizara ya Afya ya Kenya imerejesha tena utaratibu wa kuvaa barakoa katika maeneo ya umma yakiwemo supamaketi, masoko ya wazi, kwenye ndege, treni na vyombo vya usafiri wa umma ili kuzuia kuenea zaidi kwa maambukizi ya UVIKO-19.

Akitoa agizo hilo mbele ya wanahabari jijini Nairobi, waziri wa Afya  Bw. Mutahi Kagwe amesema maeneo mengine ambayo watu wanapaswa kuvaa barakoa ni pamoja na maofisini, nyumba za ibada na kwenye mikutano ya kisiasa inayofanyika nje. Waziri Kagwe amesema kiwango cha maambukizi ya UVIKO-19 nchini Kenya kimekuwa na ongezeko la wastani wa asilimia 0.6 kwa wiki mwanzoni mwa Mei hadi wastani wa asilimia 10.4, hivyo amesisitiza kuwa kuna haja ya kuchukua hatua kali ili kuzuia shinikizo kwenye mfumo wa afya wa Kenya.

Bw. Kagwe amebainisha kuwa serikali itaharakisha utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 ili kuepusha watu wengi kulazwa na vifo, na kwamba maambukizi mengi mapya ni ya watu wenye dalili ndogo na kwa sasa wanatibiwa majumbani chini ya mpango unaofadhiliwa na serikali.