Viongozi wa Afrika watoa wito wa kusitisha mapambano mara moja nchini DRC
2022-06-21 09:48:39| CRI

Viongozi wa Afrika jana Jumatatu walitoa wito wa kusitisha mara moja mapambano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo yamesababisha watu kupoteza maisha na mali zao pamoja na wengi kukimbia makazi yao.

Viongozi kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan Kusini, Burundi na Tanzania wameyataka makundi yenye silaha kuondoka kwenye maeneo wanayoyashikilia, na kusisitiza kuwa mchakato wa amani unapaswa kuimarishwa na pande zote ili kuruhusu raia wa DRC kujihisi salama na kuweza kuinuka na kuendelea na shughuli zao za kijamii, kiutamaduni na kiuchumi.

Viongozi hao waliokuwa kwenye Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wa mazungumzo baina ya watu wa Congo ya mchakato wa Nairobi juu ya hali ya amani na usalama mashariki mwa DRC, walitoa wito kwamba lugha zote za kuudhi, kauli za chuki, vitisho vya mauaji ya kimbari na lugha nyingine za uchochezi wa kisiasa lazima ziachwe na kupingwa na pande zote.