Miezi mitatu ya mapigano katika jimbo la DRC yasababisha watu wasiopungua 158,000 kupoteza makaazi
2022-06-24 09:05:40| CRI

Ghasia zilizozuka tangu Machi zimewakosesha makazi takriban watu 158,000 katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) jana ilisema wengi wa waliokimbia makazi yao ni wanawake na watoto kutoka maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo huko Kivu Kaskazini, mpakani mwa Uganda na Rwanda.

Ofisi hiyo ilisema mamlaka za huko ziliripoti kwamba takriban raia 13, wakiwemo watoto wanne, waliuawa wakati wa mapigano huko Rutshuru mapema wiki hii. Vijiji kadhaa katika eneo hilo havina watu. Waliokimbia makazi yao wanajihifadhi katika makanisa, shule na maeneo mengine ya muda, na wengine maelfu kadhaa kuchukuliwa na familia za wenyeji.

Licha ya vikwazo vilivyopo, mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali yanaendelea kutoa misaada ya kibinadamu katika maeneo ya Rutshuru na Nyiragongo, ambapo chakula kimesambazwa, na huduma za afya, maji na huduma za usafi zimeanza kupatikana tangu Machi.