Mashindano ya 21 ya "Daraja la Kichina" ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kenya yafanyika Nairobi
2022-07-01 21:08:33| cri

Mashindano ya 21 ya "Daraja la Kichina" ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kenya  yalifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Kaulimbinu ya mashindano hayo ikiwa ni “dunia moja, familia moja”. Jumla ya wanafunzi 15 kutoka taasisi za Confucius chini ya vyuo vikuu vinne vya umma nchini Kenya, ambavyo ni Moi, Kenyatta, Egerton na Nairobi, walishiriki katika shindano hilo.

Wakiwa wamevalia mavazi ya kifahari, washiriki waliwavutia waamuzi kwa ustadi wao wa kuzungumza kichina, kuimba nyimbo za kitamaduni za Kichina, densi na sanaa.

Waziri mshauri katika Ubalozi wa China nchini Kenya Bw. Zhao Xiyuan, anasema kuwa shindano hilo la ujuzi wa lugha ya Kichina limetoa jukwaa la kukuza uhusiano na urafiki wa kitamaduni kati ya China na Kenya, na kuongeza kuwa lugha na utamaduni vinasalia kuwa nyenzo muhimu za kujenga ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Naibu Chanzela wa Chuo Kikuu cha Nairobi Stephen Kiama, amepongeza mawasilisho ya wanafunzi na akiyataja kuwa ishara wa kuongezeka kwa uhusiano wa lugha na utamaduni wa Kichina.

Anasema kusoma lugha ya kichina, kunawapa vijana fursa nzuri ya kupata ajira kwenye kampuni na mashirika ya wachina.  

Baada ya karibu masaa manne ya kushindana Hansnick Omondi mwenye umri wa miaka 22 katika Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi alitangazwa mshindi.