Watu 338 wauawa katika mashambulizi ya hivi karibuni nchini Ethiopia
2022-07-01 08:43:30| CRI

Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Billene Seyoum amesema, takwimu alizopokea kutoka mkoa wa Oromia mpaka kufikia jumatano zilithibitisha kuwa, watu 338 wameuawa katika shambulizi la hivi karibuni lililofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa waasi wa kundi la Harakati za Ukombozi wa Oromo (OLA).

Amesema kufuatia shambulizi hilo, serikali imeongeza operesheni zake za usalama dhidi ya waasi wa kundi hilo, na kuongeza kuwa, amani na usalama wa Ethiopia unakabiliwa na tishio kutoka nguvu za ndani na nje ya nchi hiyo.

Serikali ya Ethiopia na watu walionusurika katika shambulizi hilo wamewashutumu wapiganaji wa kundi la OLA kwa kufanya shambulizi hilo, tuhuma ambazo kundi hilo limezipinga.

Shambulizi la silaha dhidi ya wakulima wa jamii ya Amhara lililotokea Juni 18 katika eneo la Tole wilaya ya Gimbi kanda ya Wollega Magharibi mkoani Oromia liliripotiwa kusababisha idadi kubwa ya vifo.