Umoja wa Afrika wasema COVID-19 ni changamoto kubwa kwa utekelezaji wa eneo la soko huria
2022-07-06 08:58:26| CRI

Umoja wa Afrika umesema janga la COVID-19 limekuwa changamoto kubwa kwenye utekelezaji wa makubaliano ya eneo la biashara huria la Afrika (AfCFTA).

Taarifa iliyotolewa mjini Addis Ababa kabla ya mkutano kuhusu maendeleo ya viwanda barani Afrika, inasema janga la COVID-19 limeongeza changamoto kwenye mazingira ya biashara, kwa kukatisha minyororo ya usambazaji duniani, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya viwanda.

Hata hivyo taarifa imesema changamoto hiyo pia ni fursa kwa Umoja wa Afrika kupanga vizuri vipaumbele vyake vinavyoweza kuchochea maendeleo ya viwanda.

Taarifa pia imesema kuendeleza minyororo ya thamani ya kikanda, kunaweza kutoa mchango mkubwa katika kujenga makampuni madogo na yenye ukubwa wa kati yaliyohimilivu, na kutumia fursa zilizoletwa na kukatika kwa mnyororo wa usambazaji duniani kutokana na janga la COVID-19.