UM waonya kuhusu hatari zaidi ya njaa nchini Somalia kutokana na ukame mkali
2022-07-06 09:17:29| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu (OCHA) imeonya kuhusu hatari ya kuongezeka kwa baa la njaa nchini Somalia baada ya mfululizo wa misimu minne duni ya mvua tangu mwaka 2020.

Ripoti moja iliyotolewa hivi karibuni na ofisi hiyo, imesema wasomali zaidi ya milioni 7 wanakabiliwa na njaa kali. Japo washirika wa kibinadamu wameimarisha juhudi za kusambaza misaada kwa waathirika wa maafa ya ukame, lakini wamekumbwa na uhaba wa raslimali na tatizo la kuwafikia.

Tangu Januari mwaka huu, watoto wasiopungua 200 wamefariki kutokana na utapiamlo na magonjwa nchini humo.

Ripoti pia imesema, dola milioni 993.3 za kimarekani zinahitajika haraka ili kutekeleza mpango wa kukabiliana na ukame na kuzuia baa la njaa kuwasaidia watu milioni 6.4 wenye mahitaji nchini humo kabla ya mwezi wa Desemba.