“Maharagwe ya China” yaleta “lishe bora” Tanzania
2022-07-06 14:57:38| CRI

Julai Mosi mwaka huu, mradi wa “maharagwe madogo, lishe bora” uliotekelezwa na timu ya utafiti wa maendeleo ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha China ulikamilisha mafunzo katika vijiji vinne vya kielelezo ambavyo ni Mtego wa Simba, Makuyu, Kitete na Peapea mkoani Morogoro. Miezi ya Juni na Julai kila mwaka huwa ni msimu wa mavuno ya maharagwe ya soya nchini Tanzania. Mafunzo hayo yaliyofanyika katika msimu huo, yalilenga kuwafundisha wanavijiji wa huko ustadi wa kutengeneza maziwa ya soya na bidhaa nyingine za soya. 

Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Uchumi na uzalishaji mkoani Morogoro, Dk. Rozalia Rwegasira, ambaye alitembelea China mara nyingi na kuwahi kuonja maziwa ya soya mwenyewe, alijitolea kuwafundisha wanavijiji mkono kwa mkono namna ya kutengeneza maziwa ya soya. Anaona maziwa hayo ni bidhaa nzuri, na anatumai kuwa mradi huu wa maharagwe ya soya utaweza kuwanufaisha watu wengi zaidi, wakiwemo watoto wenye umri chini ya miaka mitano, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha. Dk. Rwegasira anaamini kuwa uuzaji wa bidhaa za maharagwe ya soya utasaidia kuongeza mapato ya wakulima. Pia amesema serikali ya mkoa wa Morogoro itaimarisha mawasiliano na timu ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha China na serikali za mitaa, ili kuunga mkono na kusukuma mbele ushirikiano huo wa kilimo. 

Bw. Adam Hassan Tumbo mwenye umri wa miaka 61 ni mwanakijiji wa kijiji cha Kitete, alipewa sifa ya “mkulima bora wa maharagwe ya soya mwaka 2022”. Bw. Tumbo ameamua kupanua eneo la upandaji wa maharagwe ya soya hadi kufikia hekta moja, baada ya kuonja maziwa ya soya. 

Mradi wa “Maharagwe Madogo, Lishe bora” ni mradi mwingine wa kupunguza umaskini na kuhimiza maendeleo ya vijijini nchini Tanzania uliotekelezwa na timu ya utafiti wa maendeleo ya Afrika ya Chuo Kikuu cha Kilimo cha China baada ya timu hiyo kukamilisha mradi wa “Teknolojia Ndogo, Mavuno Makubwa”(Simple Technology, Big Harvest) nchini humo ulioanza mwaka 2011. Kuanzia mwaka 2011, profesa Li Xiaoyun wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha China aliongoza timu hiyo kwenda kwenye maeneo ya vijijini mkoani Morogoro, ili kueneza teknolojia ya kuongeza tija katika uzalishaji wa mahindi. Katika muongo uliopita, wanufaika wa teknolojia hiyo wameongezeka kutoka mkulima mmoja katika kijiji kimoja hadi kufikia maelfu ya wakulima kote mkoani humo, na teknolojia hiyo imefanikiwa kuongeza mara mbili hadi tatu uzalishaji wa mahindi, na kuleta mavuno mengi kwa wakulima maskini nchini Tanzania. 

Juhudi za timu ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha China hazikuishia hapa. Kutokana na wakulima wengi wa Tanzania kukosa fedha za kununua mbolea, upandaji wa mahindi kwa muda mrefu unaweza kupunguza rutuba kwenye ardhi. Kuanzia mwaka 2021, timu hiyo na washirika wao wenyeji walizindua majaribio ya kilimo mseto cha mahindi na maharagwe ya soya( maize/soybean intercropping). Ikiwa ni sawa na teknolojia ya kuongeza tija ya uzalishaji wa mahindi, kilimo mseto cha mazao hayo mawili pia ni teknolojia ya jadi ya kilimo ya China, maharagwe ya soya si kama tu yanasaidia kurutubisha udongo, bali pia yanaboresha lishe kwa wakulima, na makapi ya maharagwe yanaweza kutumika kama mbolea. Mradi wa “Maharagwe Madogo, Lishe Kubwa” umethibitisha mara nyingine kuwa, teknolojia nyingi za kilimo kama hizo zilizotekelezwa vizuri nchini China pia zina mustakbali mzuri wa kuenezwa katika sehemu nyingine barani Afrika.