Tanzania yapanga kujenga chuo kikuu kwa ajili ya kufundisha Kiswahili
2022-07-08 09:04:04| CRI

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Bw. Mohammed Mchengerwa ametangaza kuwa Tanzania inapanga kujenga Chuo kikuu maalumu kwa ajili ya kufundisha lugha ya Kiswahili. Bw. Mchengerwa alitoa taarifa hiyo wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili mjini Dar es Salaam.

Bw. Mchengerwa amesema serikali imetenga ardhi ya hekta 100 kwa ajili ya ujenzi huo, na wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na maofisa waandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO) watakutana wiki ijayo kujadili mambo husika.

Kutokana na ujumbe wa mkurugenzi mkuu wa UNESCO Bi. Audrey Azoulay, lugha ya Kiswahili ina zaidi ya wazungumzaji milioni 200 duniani na ni moja ya lugha za Afrika zinazotumiwa na watu wengi.  Tarehe 7 Julai ya kila mwaka imetambuliwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili.