Jeshi la Uingereza laanza zoezi la kuondoa mabomu ambayo hayakulipuka baada ya mazoezi nchini Kenya
2022-07-11 10:41:00| CRI

Shirika la Utangazaji la Kenya KBC limeripoti kuwa Kitengo cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya (Batuk) kimeanza zoezi kubwa la kuondoa mabomu ambayo hayajalipuka na risasi zilizoachwa katika viwanja vyao vya mafunzo vilivyokuwepo huko kaunti za Laikipia na Samburu ikiwa ni juhudi ya kuhakikisha maeneo hayo yanakuwa salama kwa binadamu, mifugo na wanyama pori.

Akizungumza katika Kiwanja cha Mafunzo ya Upigaji Mishale huko Kaunti ya Samburu, naibu kamanda wa Batuk nchini Kenya Luteni Kanali Finlay Bibby alisema kuwa uondoaji wa vifaa vyote vya kijeshi katika maeneo ambayo mazoezi ya kijeshi yalifanyika ni ushirikiano wa pamoja na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).

Hatua hiyo imekuja baada ya kesi ya kisheria iliyowasilishwa katika mahakama ya London mwaka 2002 na wakili wa Uingereza, akisaidiwa na wanaharakati, ambapo mahakama ya Uingereza ilitoa fidia ya zaidi ya dola za kimarekani milioni saba kwa watu wa jamii ya Wamasai katika wilaya za Laikipia na Samburu. Kwa miongo kadhaa, mabomu yaliyoachwa na jeshi la Uingereza katika maeneo yao ya malisho yaliwajeruhi binadamu, mifugo na wanyamapori.