Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania aahidi kuimarisha vita dhidi ya uhalifu wa mtandaoni
2022-07-11 10:30:48| CRI

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Simon Sirro ameahidi kuimarisha vita dhidi ya uhalifu wa mtandaoni nchini humo, akisisitiza kuwa polisi wanapaswa kuhakikisha usalama wa watumiaji wa mifumo ya kompyuta na Tehama dhidi ya mashambulizi ya mtandaoni.

IGP Sirro amesema hayo wakati alipotembelea banda la Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa, Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Ameongeza kuwa polisi wakishirikiana na TCRA wameweka hatua ambazo zitahakikisha kuwa mtu yeyote anayetenda uhalifu wa mtandaoni anapatikana, kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano wa TCRA Bw. Semu Mwakyanjala amesema mamlaka hiyo inatoa elimu kwa wananchi kuhusu jinsi ya kuripoti mashambulizi ya mtandaoni.