DRC yawa mwanachama kamili wa saba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
2022-07-12 10:31:26| CRI

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) jana Jumatatu imekuwa mwanachama kamili wa saba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baada ya kukabidhi nyaraka za uthibitisho wa kuingia kwenye mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.

Mwezi Disemba, mkutano wa 18 wa kilele wa wakuu wa nchi za EAC, uliliagiza Baraza la Mawaziri wa EAC kuanza na kukamilisha mazungumzo na DRC ya kuingia mkataba wa kujiunga kikamilifu kwenye jumuiya hiyo.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema kuingia kwa DRC kwenye jumuiya ya EAC itakuwa hatua mpya kwenye mafungamano yao, na kusisitiza kwamba Tanzania imeazimia kushirikiana kwa karibu na wanachama wote wa EAC ili kuupeleka ushirikiano huo katika ngazi ya juu zaidi. Naye rais Paul Kagame wa Rwanda amekaribisha hatua zilizopigwa katika kuiingiza DRC kwenye jumuiya hiyo ya kikanda.

Jumuiya ya Afrika Mashariki inajumuisha nchi za Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Uganda na DRC.