Vibweta vitupu vya risasi zaidi ya 130 vyagunduliwa kwenye eneo la tukio la ufyatuaji risasi Johannesburg
2022-07-12 10:32:29| CRI

Waziri wa Kipolisi nchini Afrika Kusini Bheki Cele jana Jumatatu alisema polisi imegundua vibweta vitupu vya risasi aina ya AK47 zaidi ya 130 kwenye eneo la tukio la ufyatuaji risasi lililotokea kwenye baa moja mjini Johannesburg, ambalo limesababisha watu 15 kuuawa na wengine wanane kujeruhiwa.

Akiongea na wanajamii na wanahabari nje ya baa iliyotokea shambulizi hilo, Bw. Cele amebainisha kuwa hiyo inamaanisha kwamba washambuliaji walinuia kwenda kuua. Kikundi cha watu waliobeba bunduki na bastola waliingia kwenye baa saa 6:30 Jumapili usiku kwa saa za huko na kuanza kuwafyatulia risasi wateja waliokuwa wamekaa ndani, na kuua watu 12 papo hapo kwenye eneo la tukio huku wakiwajeruhi wengine 11, ambapo kati yao watatu walifariki baadaye.

Bw. Cele amesema amekusudia kusambaza polisi wengi zaidi kufanya doria na kuwatafuta watu wanaomiliki silaha kiharamu kwenye jamii za wenyeji. Hadi sasa sababu ya shambulizi hilo haijajulikana.