Kenya na UNICEF wasambaza chakula tiba ili kuzuia utapiamlo kwa watoto
2022-07-13 10:33:12| CRI

Wizara ya Afya ya Kenya na Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) Jumanne walisambaza chakula tiba kwenye kaunti nne zilizokumbwa na ukame ili kusaidia kukinga utapiamlo mkali kwa watoto.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na UNICEF jijini Nairobi, shehena yenye chakula cha lishe ya hali ya juu ambacho kina thamani ya shilingi milioni 30 sawa na dola za kimarekani 253,915, ni sehemu ya juhudi za kupunguza hali mbaya ya ukame kwa afya ya watoto na usalama wa lishe.

Miongoni mwa kaunti zenye ukame ambazo zitanufaika na chakula hicho ni pamoja na Turkana, Mandera, Wajir na Isiolo zilizopo kaskazini mwa Kenya. Kupitia mfuko wa UNICEF, wizara ya afya imeweza kununua, kuhifadhi na kutoa chakula kama vile maziwa katika kaunti 25 zinazopambana na utapiamlo.