CEMAC yaridhishwa na uwazi ulioonyeshwa kwenye uchaguzi wa wabunge, mameya na madiwani nchini Jamhuri ya Congo
2022-07-14 11:08:33| CRI

Tume ya Waangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Kiuchumi na Fedha ya Afrika ya Kati (CEMAC) imesema imeridhika na chaguzi za wabunge, mameya na madiwani zilizofanyika nchini Jamhuri ya Congo.

Kwenye taarifa yake tume hiyo pia imeeleza kuridhishwa na uwazi uliokuwepo katika kuhesabu kura na kutangaza sehemu ya matokeo ya uchaguzi kwenye vituo vya kupigia kura. CEMAC ilipeleka waangalizi wake katika idara mbalimbali nchini humo ambapo waliangalia mwenendo wa kazi, na kuona kwamba hakukuwepo na matukio makubwa, kazi zimefanyika katika mazingira ya amani, na kuheshimu sheria za demokrasia. Sambamba na hilo tume hiyo imeishauri serikali ya Jamhuri ya Congo kuimarisha mazingira ya amani wakati wa kipindi cha uchaguzi na kuongeza uelewa wa watu juu ya vurugu za uchaguzi.

Aidha tume hiyo imevitaka vyama vya siasa na wagombea wa uchaguzi kupeleka wawakilishi wao kwenye vituo vya kupigia kura, kabla ya kuwaalika wanahabari kutekeleza jukumu lao kutoa habari sahihi kwa umma kwa njia isiyo na upendeleo. Watu milioni 2.8 wa Congo walipiga kura Julai 10 ili kuchagua wabunge, mameya na madiwani.