IGAD kutuma ujumbe kuangalia uchaguzi wa Kenya
2022-07-15 09:33:24| CRI

Katibu mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) Workneh Gebeyehu jana alisema shirika hilo litatuma ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi nchini Kenya ili kuangalia uchaguzi wa nchi hiyo utakaofanyika tarehe 9 mwezi Agosti.

Gebeyehu alitoa taarifa akisema ujumbe huo wa waangalizi utaongozwa na rais wa zamani wa Ethiopia Mulatu Teshome, ambaye ni mwanasiasa anayeheshimiwa na mwanadiplomasia aliyebobea. Hata hivyo taarifa hiyo haikutaja tarehe ya kuwasili kwa ujumbe huo.

Shirika la IGAD linaloundwa na nchi zikiwemo Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda limesema ni heshima kubwa kualikwa na tume ya uchaguzi ya Kenya, na linapenda kuendelea kushirikiana na watu wa Kenya, taasisi za uchaguzi, viongozi wa kisiasa, na timu nyingine za waangalizi, ili kuhimiza mchakato wa demokrasia.