UM watenga dola za kimarekani milioni 15 kuwasaidia watu wanaokabiliwa na njaa Jamhuri ya Afrika ya Kati
2022-07-20 08:50:42| CRI

Mratibu wa Masuala ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ameridhia kutolewa kwa dola za kimarekani milioni 15 ili kuwasaidia watu 200,000 wanaokabiliwa na uhaba wa chakula nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Naibu msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema, Griffiths ametenga fedha hizo kutoka Mfuko wa Mahitaji ya Dharura wa Umoja wa Mataifa. Amesema watu wengi wanaishi kwenye maeneo yenye mapigano, ambako hali mbaya ya usalama na watu kukimbia makazi yao vimepunguza upatikanaji wa ardhi ya kilimo, na kuzuia watu kufikia masoko.

Msemaji huyo amesema, makadirio ya kuongezeka kwa bei ya chakula kwa asilimia 70 itakapofika mwezi ujao kutokana na hali mbaya ya hewa na mapigano vimeifanya hali nchini CAR kuwa mbaya zaidi.