Kenya yapunguza bei ya unga wa mahindi kukabiliana na njaa
2022-07-21 08:41:09| CRI

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema serikali yake imepunguza bei ya unga wa mahindi kwa nusu, ili kuwaepusha wananchi kukumbwa na uhaba wa chakula unaosababishwa na ukame wa muda mrefu na kupanda kwa bei ya mafuta.

Rais Kenyatta amesema hayo alipokutana na waandishi wa habari. Amesema mfuko wa kilo mbili wa unga wa mahindi utauzwa kwa shilingi 100, sawa na dola za kimarekani senti 84 kutoka dola 1.73. Amesema uamuzi wa kupunguza bei ya unga wa mahindi, ambao ni chakula kikuu nchini humo, unalenga kuepusha watu kuathiriwa na njaa na utapiamlo.

Hivi sasa zaidi ya Wakenya milioni 4.1 wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula, kutokana na upungufu wa mvua katika misimu minne ya mvua kwa mfululizo, uvamizi wa nzige wa jangwani, mzozo wa Ukraine na janga la COVID-19.