Washirika wa kibinadamu watalazimika kusitisha msaada kwa Somalia kutokana na ukosefu wa fedha
2022-07-25 08:40:27| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya jana jumapili kuwa, washirika wa kibinadamu watalazimika kusitisha msaada kwa Somalia kutokana na ukosefu wa fedha.

Kwa mujibu wa OCHA, bila ya fedha kupatikana mara moja, programu za misaada kama vile chakula, lishe na huduma za afya, zitasitishwa.

Kwenye ripoti yake mpya juu ya gharama ya kutochukua hatua iliyotolewa mjini Mogadishu, OCHA imesema kuwa wasomali wengi zaidi wataathirika, na maendeleo yaliyopatikana katika muongo uliopita yataweza kupotea.

Shirika hilo pia limeonya kuwa hali mbaya ya ukame nchini Somalia imeathiri watu milioni 7.7, ikiwa ni nusu ya watu wote wa nchi hiyo, ambao wanahitaji msaada wa kibinadamu au ulinzi.