Watoto 11 wafariki katika ajali ya barabarani Tanzania
2022-07-27 08:51:19| CRI

Watu wasiopungua 13, wakiwemo watoto 11 wa shule ya chekechea na msingi, wamefariki na wengine 16 kujeruhiwa Jumanne asubuhi baada ya basi la shule walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kutumbukia kwenye shimo mkoani Mtwara kusini mwa Tanzania.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara Bw. Nicodemus Katembo amesema ajali hiyo ilitokea saa moja asubuhi kwa saa za huko kwenye eneo la Mikindani pembezoni mwa mji wa Mtwara baada ya breki kugoma wakati basi hilo lilipokuwa njiani kuwapeleka watoto shule.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi kwa mkuu wa mkoa wa Mtwara Marco Gaguti kwa niaba ya familia za wafiwa, akisema alishtushwa na msiba wa watoto hao.