Askari mmoja wa kulinda amani na polisi wawili wauawa DRC
2022-07-27 08:56:39| CRI

Askari mmoja wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na askari polisi wengine wawili wameuawa na mmoja kujeruhiwa kufuatia kuongezeka kwa vurugu nchini humo.

Ripoti ambazo bado hazijathibitishwa zimesema raia kadhaa pia wameuawa wakati wa maandamano ya kupinga kikosi cha kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika kambi ya Kikosi hicho iliyoko Butembo, mkoa wa Kivu Kaskazini.

Naibu msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema washambuliaji waliwanyang’anya silaha askari polisi wa DRC na kuwafyatulia risasi askari wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa.

Amesema kulikuwa na matukio manne yaliyolenga makazi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini DRC na makazi ya wafanyakazi wengine, na kuongeza kuwa kundi la watu lilijaribu kuingia kwa nguvu katika uwanja wa ofisi za Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa zilizoko Goma, lakini walizuiwa na walinzi waliokuwepo kwenye eneo hilo.