Rais Kenyatta azindua rasmi barabara ya Nairobi Expressway iliyojengwa na kampuni ya China
2022-08-01 09:30:02| CRI

Rais Kenyatta wa Kenya Jumapili alizindua rasmi barabara ya Nairobi Expressway iliyojengwa na Kampuni ya Barabara na Madaraja ya China (CRBC), akisema barabara hiyo itasaidia sana kutatua tatizo la msongamano wa magari jijini Nairobi.

Rais Kenyatta alitoa mfano akisema sasa inachukua kati ya dakika 15 na 24 kuendesha gari kutoka Mlolongo katika Kaunti ya Machakos hadi Rironi katika Kaunti ya Kiambu, lakini kabla ya kufunguliwa kwake, safari hiyo ilichukua saa tatu ambazo ni sawa na kusafiri kwa ndege hadi Addis Ababa na kurudi. Pia alisema barabara hiyo itaweka mazingira mazuri zaidi ya biashara, na kuiletea Kenya fursa nyingi kwenye sekta za utalii, mikutano na hoteli.

Naye waziri wa uchukuzi na miundombinu wa Kenya Bw. James Macharia alisema barabara ya Nairobi Expressway ni mradi wa mfano wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Kwa upande wake, balozi wa China nchini Kenya Bw. Zhou Pingjian alisema China inaisaidia Kenya kutatua suala la ukosefu wa miundombinu, na kuiletea Kenya vigezo, teknolojia, usimamizi na vifaa vya China, hali ambayo inawanufaisha watu na serikali ya Kenya.