Chama cha ANC cha Afrika Kusini chaazimia kuzidi kujijenga upya
2022-08-01 09:31:15| CRI

Chama tawala cha Afrika Kusini (ANC) kimesema kuna haja ya kuzidi kujijenga upya “kiuhalisi” na kujenga taifa lenye “uwezo”, maadili na maendeleo ili kuondoa changamoto nyingi zinazowakabili watu.

Akihutubia kwenye ufungaji wa Mkutano wa Sita wa Sera za Taifa wa ANC huko Johannesburg, rais Cyril Ramaphosa amesema kuna makubaliano ya pamoja kwamba ANC na serikali lazima zishughulikie vya kutosha, kwa haraka na kwa uthubutu changamoto zinazowakabili watu katika maisha ya kila siku. Ametaja changamoto hizo zikiwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, umasikini, uhalifu, ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake. Nyingine ni ufisadi, mshikamano wa kijamii ubaguzi wa rangi, msukosuko wa nishati na kuongezeka kwa gharama za maisha.

Mkutano wa Sera za Taifa ambao umeitishwa kabla ya Mkutano wa 55 wa Taifa wa ANC, unaotarajiwa kufanyika Disemba, ulilenga kupitia sera za ANC na kupendekeza sera mpya au kuzifanyia marekebisho.