EAC yaanzisha tume ya kuangalia uchaguzi mkuu wa Kenya
2022-08-02 09:43:36| CRI

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeanzisha tume ya uchaguzi itakayofanya kazi ya kuangalia uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti 8.

Jakaya Mrisho Kikwete, mkuu wa tume hiyo ya waangalizi wa uchaguzi wa Kenya, aliwaambia wanahabari jijini Nairobi kuwa timu yake ina watu 52 kutoka taasisi muhimu za serikali na huru za mataifa wanachama pamoja na mashirika ya kiraia. Amesema, wanaona kwamba uangalizi wa kikanda ni muhimu ili kuzidisha uaminifu wa uchaguzi, kuongeza nguvu ya makundi ya waangalizi wa ndani, na kuimarisha imani ya umma katika mchakato mzima wa uchaguzi. Rais huyo mstaafu wa Tanzania amesema tume ipo nchini Kenya kuanzia jana Agosti mosi na itaendelea kuwepo hadi Agosti 12 ili kuangalia shughuli za maandalizi ya uchaguzi.

Uchaguzi huo unawapambanisha wagombea kutoka vyama viwili vikubwa vya muungano wa kisiasa ambavyo ni Kenya Kwanza kinachoongozwa na naibu rais William Ruto na Azimio la Umoja kinachoongozwa na Waziri Mkuu Raila Odinga ambaye anaungwa mkono na rais Uhuru Kenyatta.