UM yatoa ufafanuzi zaidi kuhusu ghasia za walinda amani nchini DR Congo
2022-08-03 09:27:27| CRI

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Bw.  Stephane Dujarric amesema kuwa Umoja wa Mataifa umetoa ufafanuzi zaidi kuhusu tukio la mauaji lililotokea Jumapili huko Kasindi katika jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC, ambalo linawahusisha walinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Walinda amani waliokuwa wanatoka likizo na kurejea nchini DRC waliwaua raia wawili baada ya awali kukataliwa kuingia nchini humo. Taarifa za awali zilionyesha wanajeshi hao walisubiri usiku kucha katika eneo kati ya kituo rasmi cha kutoka Uganda na kituo rasmi cha kuingia DRC. Walinda amani hao wanadaiwa kuwaua raia wawili kwa risasi na kuwajeruhi wengine 15.

Ingawa Dujarric hakubainisha idadi ya walinda amani wala utaifa, amesema tume iliwasiliana na nchi husika kwa lengo la kuendeleza uchunguzi wa mahakama ya kitaifa na kwamba MONUSCO iliamuru uchunguzi ufanyike. Kuna zaidi ya walinda amani 12,000 nchini DRC kutoka nchi zaidi ya 10.