Kenya yazindua mpango wa msaada wa chakula kwa wananchi wanaokumbwa na ukame
2022-08-04 11:13:37| CRI

Kenya jana ilizindua mpango wa msaada wa chakula ili kusaidia wananchi wanaokumbwa na ukame.

Waziri wa Huduma ya Umma, Jinsia, Masuala ya Raia Wazee na Miradi Maalum wa Kenya Profesa Margaret Kobia amesema mpango huo ni kwa ajili ya familia elfu 89 zilizoko kwenye kaunti 12, ambazo zinakumbwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula. Msaada huo wa chakula utakaotolewa kwa muda wa miezi sita, utakuwa kwa njia ya fedha na  kunufaisha familia kwa kupokea shilingi 6,500 za Kenya sawa na dola 55 za kimarekani kila mwezi.

Wakati huohuo, Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) jana ilisema hali ya ukame mkali nchini Somalia imesababisha watu 918,000 kupoteza makazi yao. Ofisi hiyo imesema itaweka kipaumbele katika kuwasaidia watu wanaokumbwa na baa la njaa.