Kenya yaimarisha usalama wakati ikielekea kwenye uchaguzi
2022-08-09 08:32:48| CRI

Jeshi la Polisi nchini Kenya limesema limeimarisha usalama nchini humo ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unaofanyika leo, unafanyika kwa amani.

Msemaji wa Jeshi hilo Brumo Shioso amesema, zaidi ya maofisa usalama 150,000 kutoka Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS), Jeshi la Magereza, Shirika la Wanyamapori la Kenya (KWS), na Huduma ya Wanyamapori nchini humo wamepelekwa kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ili kuhakikisha usalama wakati wa kupiga kura.

Amesema askari hao wamejengewa uwezo na wako tayari kukabiliana na aina zote za vitisho vinavyoweza kutokea kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), Wakenya milioni 22.1 leo wanapiga kura katika uchaguzi wa tano wa rais, wabunge, maseneta, na magavana wa kaunti.