Wakenya wapiga kura katika uchaguzi mkuu
2022-08-10 08:41:07| CRI

Mamilioni ya Wakenya jana jumanne wamejitokeza kupiga kura katika vituo 46,229 nchini humo ambapo wanatarajiwa kuchagua rais wa awamu ya tano, pamoja na wabunge, maseneta na magavana wa kaunti.

Naibu rais wa Kenya William Ruto ambaye anagombea nafasi ya urais kupitia Muungano wa Kenya Kwanza, alipiga kura saa kumi na mbili kwa saa za huko katika shule ya msingi kijijini kwake Sugoi katika kaunti ya Uasin Gishu, ambapo mara baada ya kupiga kura hiyo, Ruto alisema ataheshimu matokeo ya uchaguzi.

Ruto anagombea nafasi hiyo pamoja na wagombea wengine watatu, akiwemo mpinzani wake mkubwa Raila Odinga anayegombea nafasi hiyo kupitia Muungano wa Azimio la Umoja alipiga kura katika shule ya msingi iliyoko mtaa wa mabanda wa Kibera.

Wagombea wengine wa nafasi hiyo ni George Wajackoya anayegombea chini ya chama cha Roots na David Waihiga anayewakilisha chama cha Agano.