Makamu mwenyekiti wa baraza la utawala nchini Sudan aahidi kuweka wazi njama dhidi ya masikilizano ya kikabila
2022-08-11 08:31:09| CRI

Makamu mwenyekiti wa Baraza la Utawala wa Mpito la Sudan Mohamed Hamdan Daqlu ameahidi kuweka wazi njama ovu dhidi ya masikilizano kati ya makabila nchini humo.

Akizungumza na wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa mjini Khartoum, Bw. Daqlu amesema Baraza hilo lina taarifa za njama hizo, na litaweka wazi watu wanaohusika na mipango hiyo.

Amerejea tena ahadi ya serikali ya kukabiliana na mapigano ya kikabila na kupendekeza maridhiano kati ya makabila katika sehemu ya kaskazini mwa mkoa wa Darfur na nchi jirani ya Chad. Amesema ni muhimu kudumisha amani katika mpaka na Chad ili kuzuia kutokea tena kwa kile kinachoitwa mashambulizi ya kuvuka mpaka yanayofanywa na makundi yenye silaha kutoka Chad yaliyosababisha vifo vya raia 18 wa Sudan tarehe 4 mwezi huu.