Watu 21 wauawa katika shambulizi la hoteli ya Hayat, nchini Somalia
2022-08-22 10:26:23| CRI

Serikali ya Somalia imethibitisha kwamba watu 21 waliuawa na wengine 117 kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi lililotokea kwenye hoteli moja maarufu ya Hayat katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu Ijumaa jioni.

Waziri wa Afya ya Somalia Bw. Ali Haji Adan amesema watu 15 walijeruhiwa vibaya na wako mahututi baada ya washambuliaji kufyatua vilipuzi na kuvilipua wakiwa wanaelekea ndani ya hoteli hiyo huku wakivikabili vikosi vya usalama katika mapigano ya kurushiana risasi yaliyodumu kwa saa 30.

Awali, Kamishna wa Polisi Bw. Abdi Hassan Mohamed alisema kuwa vikosi maalumu vya ulinzi na usalama vilijikita zaidi katika kuwaokoa watu waliokuwa kwenye hoteli hiyo wakati operesheni ikifanyika, na kubainisha kuwa watu 106 wakiwemo wanawake na watoto waliokolewa.