Mradi mkubwa wa umeme wa maji katika Afrika Mashariki wakaribia kumalizika
2022-08-22 10:21:47| CRI

Ujenzi wa mradi wa umeme wa maji ambao ni wa kikanda unaofahamika kama Rusumo Falls umeshatekelezwa kwa asilimia 95 kabla ya kuanza kufanya kazi.

Kikitolea ufafanuzi wa mradi huo, Kitengo cha Uratibu cha Kampuni Tanzu kinachoshughulikia Mpango wa Utekelezaji wa Maziwa ya Ikweta ya Nile kimesema kinashughulikia mradi huo kwa niaba ya serikali za Burundi, Rwanda na Tanzania ambazo ndio wamiliki wa mradi.

Waziri wa Miundo Mbinu wa Rwanda Ernest Nsabimana, ambaye ameliongoza baraza la mawaziri wakiwemo Waziri wa Maji, Nishati na Migodi wa Burundi Ibrahim Uwizeye na Waziri wa Nishati wa Tanzania Januari Yusuf Makamba kwenda kuangalia maendeleo ya mradi huo, amesema Jumamosi kuwa mradi wa umeme wa maji utakapokamilika utapiga jeki shughuli za uchumi, maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji katika miundombinu kupitia kuongeza upatikanaji wa umeme katika kanda hiyo.

Nchi zote tatu zinatarajiwa kupokea umeme wa megawati 26 unaounganishwa moja kwa moja kwenye gridi zao za taifa, na kunufaisha zaidi ya watu milioni moja wa nchi hizo tatu.