Raila Odinga afungua kesi kwenye mahakama ya juu akipinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Kenya
2022-08-23 09:39:15| CRI

Kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga jana Jumatatu alifungua kesi katika mahakama ya juu, akipinga matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyotangazwa wiki iliyopita na Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya Wafula Chebukati, ambapo mpinzani wake William Ruto alitangazwa mshindi.

Odinga ambaye amewania kiti cha urais kwa mara ya tano sasa chini ya Azimio la Umoja, amesema matokeo ya uchaguzi hayakuwa halali na yalikuwa na kasoro nyingi, akidai kuwa maafisa wa uchaguzi wamefanya ouvu mkubwa. Odinga na mgombea wake mwenza Martha Karua pia wamedai kuwa matokeo ya mwisho hayakukamilika na kuongeza kwamba kumekuwa na tofauti kubwa baina ya matokeo yaliyomo kwenye mashine za kieletroniki na fomu za kawaida.

Wadai wengine watatu wamefungua kesi ya kubatilisha matokeo kwenye mahakama ya juu, ambapo kesi itaanza kusikilizwa leo Jumanne huku majaji wakitarajiwa kutoa hukumu baada ya wiki mbili. Kwenye hukumu yao majaji wanaweza kuhalalisha ushindi wa Ruto, kuamuru kura zihesabiwe tena au kubatilisha matokeo na kuamuru uchaguzi ufanyike tena baada ya siku 60.