Sudan Kusini yasema iko tayari kuandaa mazungumzo kuhusu mpaka kati ya Sudan na Ethiopia
2022-08-23 09:43:16| CRI

Mshauri wa masuala ya usalama wa rais Salva Kiir wa Sudan Kusini Bw. Tut Gatluak Manime amesema kwamba rais huyo yuko tayari kuandaa mkutano wa pande tatu wa kusuluhisha mizozo ya mpaka kati ya Sudan na Ethiopia.

Tut Gatluak Manime alisema hayo wakati wa mkutano wake na Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan siku ya Jumatatu mjini Khartoum, ambapo "walipitia uhusiano wa kisiasa na masuala ya mpaka kati ya nchi hizo mbili".

Aliongeza kuwa pande hizo mbili pia zilijadili uhusiano kati ya Sudan, Sudan Kusini na Ethiopia, na kusema uhusiano wa pande hizo tatu utashuhudia kipindi kipya cha ushirikiano.

Tangu Septemba 2020, maeneo ya mpaka kati ya Sudan na Ethiopia yamekuwa yakishuhudia mivutano na mapigano mabaya ya kumwaga damu yakiongezeka kati ya majirani hao wawili.