Tanzania yafanya sensa ya watu na makazi katika nchi nzima
2022-08-24 09:29:19| CRI

Tanzania jana ilifanya Sensa ya Watu na Makazi katika nchi nzima ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mmoja wa watu wa kwanza kuhesabiwa katika Ikulu ya Chamwino iliyopo mjini Dodoma.

Timu ya maofisa wa sensa wakiongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bw. Albina Chuwa na Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Anna Makinda, walimtembelea rais saa 12 asubuhi kwa ajili ya kuhesabiwa.

Akiwatoa hofu wananchi mbele ya wanahabari, Rais Samia amesema kuwa yeye amemaliza kuhesabiwa, na ni kweli kulikuwa na maswali mengi lakini yote yanaweza kujibiwa kwa muda mfupi, na kubainisha kuwa matokeo ya awali ya sensa yatatangazwa mwezi Oktoba. Sensa ya mwisho ya Watu na Makazi ilifanyika nchini Tanzania mwaka 2012.