UM wakemea mapigano mapya katika jimbo la kaskazini nchini Sudan Kusini
2022-08-24 09:32:18| CRI

Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) imekemea mapigano mapya kati ya makundi hasimu yenye silaha katika jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini.

Kwenye taarifa yake UNMISS imeelezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa maelfu ya raia walionasa kwenye mapigano hayo na kutoa wito kwa pande zote husika kuheshimu sheria ya kimataifa na kulinda uhuru wa kuingia kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu katika eneo la Upper Nile.

UNMISS pia imesema zaidi ya watu 200 waliokimbia makazi yao wametafuta hifadhi katika eneo la Ulinzi wa Raia la UM huko Malakal, mji mkuu wa jimbo la Upper Nile, ambapo watoto wengi wameripotiwa kupotea ama kutenganishwa na familia zao.

Mapigano mapya yaliyozuka wiki iliyopita katika mji wa Tonga yamesababisha zaidi ya watu 15,000 kukimbia makazi yao, ambapo mafuriko yanazuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kufika maeneo salama, huku wengine wakitafuta hifadhi kwenye kambi za UM.