Wataalamu wasema pendekezo la Ukanda Mmoja Njia Moja limebadilisha mazingira ya maendeleo ya Afrika
2022-08-25 09:28:13| CRI

Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” (BRI) limechangia pakubwa kubadilisha nchi zinazoendelea kiuchumi za Afrika kupitia maendeleo ya miundombinu, kupunguza ukosefu wa ajira na kuboresha biashara na mengine.

Hayo yamesemwa na wataalamu na wasomi mbalimbali wakati wakiongea kwenye kongamano la siku moja lililofanyika Jumatano ya wiki hii kwa njia ya video lijulikanalo kama “Umuhimu wa Pendekezo la Ukanda Mmoja Njia Moja la China kwa Afrika”.

Akiongea kwenye kongamano hilo, mtafiti wa kujitegemea na mchambuzi wa Uganda Frederick Golooba Mutebi amesema China hainyonyi Afrika kama wanavyoona watu wa magharibi, kwa sababu yakiangaliwa maendeleo ya miundombinu ya Afrika, pendekezo hili linasaidia kuibadilisha Afrika. Anaamini kuwa China ni mchangiaji muhimu kwenye maendeleo ya miundombinu ya Afrika ambayo ni moja ya vizuizi vikubwa kwa  mageuzi ya kiuchumi barani Afrika.

Naye mkurugenzi mtendaaji wa taasisi ya Pakistan na China Mustafa Hyder Sayed amesema pendekezo hili limeleta miradi mingi kwa sababu lipo chini ya msingi wa ushirikiano na urafiki wa pamoja na sio unyonyaji.