Mkuu wa Kamisheni ya AU atoa wito wa kukomesha uadui baada ya mapambano mapya ya kijeshi kuzuka nchini Ethiopia
2022-08-25 09:29:26| CRI

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameeleza wasiwasi wake mkubwa juu ya ripoti za makabiliano mapya ya kijeshi nchini Ethiopia na kutoa wito wa kukomesha uadui, akizitaka pande husika kurejesha mazungumzo ya kutafuta suluhu ya amani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Afrika iliyotolewa Jumatano jioni, Bw. Faki amesisitiza kuwa Umoja huo unaendelea na azma yake ya kushirikiana na pande husika ili kuunga mkono mchakato wa makubaliano ya kisiasa kwa maslahi ya nchi hiyo.

Mapema Jumatano, serikali ya Ethiopia iliwashutumu waasi wa Tigray (TPLF) kwa kurejesha mapambano, na kusema makundi ya waasi yameanza kushambulia tena maeneo tofauti ya mashariki hasa Bisober, Zobil na Tekulesh.