Kenya yalenga kuuza maparachichi tani 100,000 nchini China kila mwaka
2022-08-26 09:44:38| CRI

Afisa mkuu mtendaji wa Shirika la Kuhamasisha Uuzaji Bidhaa Nje ya Nchi la Kenya (KEPROBA) Bw. Wilfred Marube amesema nchi hiyo inalenga kuuza maparachichi zaidi ya tani 100,000 nchini China kila mwaka katika miaka ijayo.

Ameongeza kuwa China inatoa fursa kwa Kenya kuongeza usafirishaji nje wa matunda pamoja na mazao mengine ya bustani. Amebainisha kuwa China ni soko kubwa kwa Kenya sio tu kwa maparachichi, bali pia kwa mazao mengine mabichi kama vile maembe na ndizi.

Alieleza kuwa soko la China litachochea uzalishaji wa maparachichi nchini Kenya na wakulima watapata kipato zaidi na pia kuongeza uwekezaji katika usindikaji wa mazao ya kilimo.

Kwa wastani, Kenya inauza nje maparachichi tani 80,000 kila mwaka, ambapo masoko makuu kwa miaka mingi yamewa ni nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na nchi za Mashariki ya Kati. Kutokana na kuanza kusafirisha matunda yake nchini China, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa.