Waziri Mkuu wa Tanzania azitaka mamlaka kuondoa changamoto zinazokabili zoezi la sensa
2022-08-26 09:47:44| CRI

Wakuu wa mikoa nchini Tanzania wametakiwa kuondoa changamoto zinazojitokeza wakati wa zoezi la sensa ya watu na makazi lililoanza Jumanne wiki hii.

Akiongea kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya video, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa aliwaambia wakuu wa mikoa hao kwamba kila mkoa unatakiwa uwe umeshakusanya takwimu za sensa za siku nzima hadi muda wa saa mbili jioni kila siku, kwani itasaidia kubaini mapungufu yanayojitokeza wakati wa zoezi hilo na kuyaondoa.

Amesema kamati za sensa za wilaya na mikoa pia zinatakiwa kufuatilia mwenendo wa sensa wakati wote kwenye maeneo yao ili kuhakikisha watanzania wote wanahesabiwa.

Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema hadi kufikia Alhamis asubuhi kaya 5,060,158 zikiwa na watu 22,004,910 zilikuwa tayari zimehesabiwa. Sensa ya Watu na Makazi ilianza Agosti 23 na itafanyika kwa siku saba ambapo inatarajiwa kukamilika Agosti 29.