Kenya na Benki ya Dunia zasaini makubaliano ya kuongeza upatikanaji wa nyumba za bei nafuu
2022-08-26 09:48:57| CRI

Shirika la Nyumba la Taifa nchini Kenya (NHC) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) ambalo ni sekta binafsi ya kukopesha fedha chini ya Benki ya Dunia, yamesaini makubaliano ya huduma za ushauri wa kifedha ili kuongeza upatikanaji wa nyumba za bei nafuu nchini humo.

Meneja wa IFC kwa Afrika Mashariki na Malawi Amena Arif, amewaambia wanahabari jijini Nairobi kuwa chini ya makubaliano hayo, IFC itasaidia kutoa shilingi bilioni 7 za Kenya (sawa na dola milioni 58.4 za kimarekani) ili kufadhili ujenzi wa nyumba 3,500 zitakazopatikana kwa bei nafuu.

Arif amebainisha kuwa Kenya inakabiliwa na upungufu wa nyumba kati ya laki mbili na laki mbili na nusu huku mahitaji ya nyumba yakizidi usambazaji, na kuongeza kuwa upanuzi wa haraka wa miji ni moja ya sababu zinazochangia uhaba wa nyumba.