Shehena ya kwanza ya parachichi kutoka Kenya yaingia katika soko la China
2022-08-29 09:03:54| CRI

Shirika la Kukuza Usafirishaji Bidhaa na Chapa la Kenya (KEPROBA) limesema, shehena ya kwanza ya parachichi kutoka nchini Kenya imeingia katika soko la China.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Wilfred Marube amesema, hatua hiyo ni ushindi mkubwa kwa Kenya kwa kuwa ina uwezekano wa kusaidia ukuaji wa uchumi wa Kenya kupitia biashara ya kimataifa ya parachichi.

Amesema safari ya Kenya ya kuuza parachichi zake nchini China ilianza mwaka 2018 kwa kusainiwa kwa makubaliano kadhaa ya awali, yakiruhusu bidhaa za kilimo za Kenya kuingia kwenye soko la China.

Balozi wa Kenya nchini China Muthoni Gichohi aliyehudhuria hafla ya kukabidhi shehena ya kwanza ya parachichi iliyofanyika Beijing, amepongeza juhudi zilizofanywa na serikali za Kenya na China katika kutimiza hatua hiyo.