Hali ya eneo la kaskazini nchini Ethiopia yatishia misaada ya kibinadamu
2022-08-30 08:34:44| CRI

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema hali katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia inaleta wasiwasi mkubwa, huku wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa wakijitahidi kuanza tena kupeleka misaada katika eneo hilo.

Amesema jumatano iliyopita, misaada ya kibinadamu ilisitishwa kupelekwa mkoani Tigray kutokana na usafiri wa ndege wa mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kushindwa kuingia ama kutoka mkoani humo tangu alhamis. 

Amesema vikwazo vimezuia usafirishaji wa fedha za matumizi na mzunguko wa wafanyakazi wa kibinadamu, na kuongeza kuwa, kuna taarifa zisizo rasmi za kuwepo kwa wakimbizi wa ndani katika maeneo ya mstari wa mbele karibu na mikoa ya Amhara na Afar.

Amesema katika mkoa wa Amhara, mamlaka zimeweka amri ya kutotembea usiku katika maeneo ya Debark, Dessie na Waldiya, na hivyo kuathiri mizunguko ya raia, upatikanaji wa huduma za afya za dharura, na biashara.